Kutana na kitasa Jerrard Mtagwa “Jellah Mtagwa” pacha wa Leodigar Tenga taifa Stars

Historia ya soka nchini Tanzania inaweza kuwa na mengi ya kuelezea ndani lakini haitaacha kugusa baadhi ya watanzania waliochangia kwa namna moja ama nyingine safari yake tangu miaka takribani 60 iliyopita kama taifa la Tanzania ambalo mpaka sasa bado linatapatapa bila kujua ni wapi mwelekeo chanya.

Wapo viongozi na wachezaji wengi wamepita katika safari hii ambayo ni vigumu na wala haiingii akilini kuacha kumtaja mlinzi wa kati wa zamani Jerrard Mtagwa maarufu kama Jellah Mtagwa aliyezaliwa mwaka 1959 na kukulia mkoani Morogoro hususani eneo la Msamvu.

Yapo mengi ya kumzungumzia Mtagwa lakini kubwa ni zaidi ni utumishi wake wa miaka kumi akiwa nahodha wa timu ya taifa ya Tanzania kwa kipindi kirefu zaidi kuliko mchezaji mwingine yoyote.
4
Alianzia elimu yake ya soka katika shule ya msingi Mwembesongo 1965-1971 kabla ya kujiunga na shule ya sekondari ya Morogoro 1972-1975 na baadaye kuajiriwa na kampuni ya madawa ya taifa akiwa afisa mauzo.

Kipaji chake katika soka kilianza kuang’ara mwaka 1969 akiwa shuleni akicheza katika timu ya shule kabla ya 1971 kuchukuliwa na timu ya daraja la kwanza ya Nyota fc wakati huo ligi daraja la kwanza ni sawa na ligi kuu akiwa na nyota mwingine ambaye ni baba yake mlinzi wa Azam fc na timu ya taifa ya Tanzania Shomari Kapombe, Salum Kapombe.

Mwaka 1973 akaanza kuitumikia timu ya taifa tena moja kwa moja akiwa nahodha ambapo msimu uliofuiata wa 1974/75 akasajiliwa na Yanga. Mambo yakaenda kombo mitaa ya twiga na Jangwani Yanga ikagawanyika na kuzaliwa Pan Africa.

Yeye Mtagwa, Adolf Rishaard, Leodigar Tenga, Muhaji Muki, Juma Pondamali Omari Kapera na wengineo wakaondoka Jangwani na kujiunga na Pan Afrika iliyokuwa ikisapotiwa na viongozi wengi wa serikali wakati huo.

Mwaka 1980 akiwa na nyota kadhaa, Juma Pondamali, Athumani Mambosasa magolikipa hao, Leopard Tasso Mukebezi, Mohamed Kajole, Adoilf Rishard, Omari Hussein(Kegan),Hussein Ngulungu, Mohamed Salim, Thuel Ally, Ahmed Amasha, Peter Tino na wengineo chini ya kocha mzalendo Stars inafanikiwa kutinga fainali za mataifa ya Afrika wakati huo timu zilikuwa 8 tu katika fainali, mlinzi wa kati (kitasa) ni Jellah Mtagwa akisaidiwa na Leodigar Tenga.

Safari ya Stars kufuzu mataifa ya Afrika fainali zilizopigwa Lagos Nigeria ilianzia katika michezo ya kufuzu ambapo ilianza kwa kuichapa Kenya(Harambee Stars) 3-1 mchezo wa kwanza kabla ya mchezo wa marudiano Stars kuichapa Harambee Stars bao 5-0 uwanja wa taifa.

Raundi ya pili Stars ilipangiwa Mauritius ambayo ilichapwa 1-0 katika mchezo wa kwanza na kukubali kichapo kingine cha bao 4-0 uwanja wa taifa jijini Dar es Salaam.
30002

Na raundi uliyofuata Stars ikakutana na Zambia Chipolopolo ambapo mchezo wa kwanza uwanja wa taifa stars ililazimishwa suluhu 0-0 lakini katika mchezo wa marudiano nchini Zambia goli la Peter Tino katika dakika za majeruhi liliisaidia Stars kupata sare ya 1-1 na hivyo kufaidika na sheria ya goli la ugenini na kutinga fainali za mataifa ya Afrika kwa mara ya kwanza na ya mwisho.

Nahodha Jella Mtagwa atakumbukwa sana kwa mchango wake mkubwa katika soka kiasi hata picha yake kutumia katika stamp za barua na vifurushi akiwa ni mchezaji pekee kutokea katika Stamp nchi Tanzania.

Jerrard Mtagwa aliacha soka mwaka 1984 kutokana na kusumbuliwa na matatizo ya goti yaliyotokana na kugongana na Michael Chabala wa Nkana ya Nigeria na kumrithisha nafasi yake Kassim Matitu.

Kwasasa Mtagwa yuko nyumbani akipigania afya yake baada ya kupatwa na matatizo ya kupooza kwa mwili (yaani kiarusi) zaidi ya miaka 10 iliyopita huku viongozi wakubwa katika vilabu vya Yanga, Pan Afrika na shirikisho la soka nchini TFF wakiendelea na hamsini zao.

Jellah Mtagwa ana mke na watoto wanne na nyumbani kwake ni Manzese Friends kona.