Bayi afunga kozi ya fifa ya utawala bora

KATIBU mkuu wa Kamati ya Olimpiki Nchini (TOC) Filbert Bayi amefunga kozi ya utawala bora iliyoendeshwa na mkufunzi wa FIFA Henry Tandau iliyokuw ainafanyika katika uwanja wa Taifa Jijini Dar es salaam.

Kozi hiyo inayosimamiwa na Kamati ya Olimpiki ilianza Mei 08 na kufungwa Mei 12 huku kukiwa na washiriki 15 kutoka klabu mbali mbali za ligi kuu na taasisi za michezo.

Akizungumza wakati wa kufunga kozi hiyo Bayi amesema kuwa hii ni kwa mara ya kwanza kwa wawakilishi kutoka klabu mbalimbali za Ligi Kuu kushiriki katika mafunzo haya ambayo ni muhimu sana kwa maendeleo ya michezo nchini.

Amesema kuwa, ana imani kubwa sana kuwa elimu hii waliyoipata wataenda kuitumia vizuri katika kuziendesha klabu zao na kuzieletea maendeleo kwani msingi mkubwa wa maendeleo ya soka ni kuwa na utawala bora.

“Elimu hii mliyoipata leo nina imani kubwa sana mtaitumia vizuri kwani wengi wenu mnatoka katika klabu za Simba, Yanga na Azam na maendeleo ya mpira wa miguu yanaletwa na utawala bora na wasiende kuweka vyeti ndani bali wanatakiwa kuvitumia kwa ajili ya manufaa ya vizazi vijavyo,”amesema Bayi.

Mkufunzi wa FIFA Henry Tandau amemshukuru Bayi kwa kuweza kukubali kuwa mgeni rasmi kaika mafunzo hayo na kumuahidi kuwa elimu hii waliyoipata wanaimani kuwa washiriki wote wataenda kuelimisha na wengine na kuleta utawala bora kwenye klabu zao.

Mafunzo hayo ya siku 5 yameratibiwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Nchini huku ikiwa ni kwa mara ya kwanza tofauti na miaka mingine kufanyika mikoani pia yameweza kuleta tija kwa washiriki kufahamu mambo mbalimbali yanayohusu michezo ikiwemo riadha.