Bolasie – Lukaku kusalia Everton ni ngumu

Lukaku kusalia Everton ni ngumu – Bolasie
Winga wa Everton Yannick Bolasie amesema klabu yake haina uwezo wa kumzuia Romelu Lukaku endapo mshambuliaji huyo kweli atakuwa anataka kuhamia katika klabu kubwa.
Lukaku mwenye umri wa miaka 23 na ambaye anaongoza kwa kufunga magoli mengi zaidi baada ya kutupia kambani magoli 21 ameonyesha kutaka kuondoka Goodison Park na kujiunga na klabu zenye nafasi ya kucheza ligi ya mabingwa Ulaya.
Bado Toffees ina matumaini ya kumbakisha mshambuliaji huyo na tayari imetoa ofa ya mkataba mpya kwa raia huyo wa Ubeleji ambayo hata hiyo imekataliwa na mshambuliaji huyo, lakini Bolasie ambaye kwasasa ni majeruhi anasema hashangazwi na dhamira ya nyota mwenzake.
Amekaririwa na Sky Sports akisema “naongea na Rom [Lukaku] kila siku na jamaa akiwa na mipango yake huwezi kumzuia.
“wachezaji wana malengo yao, kama wachezaji wanataka kucheza katika timu kubwa inawezekana na kwake Rom wakati ndio huu, kwa umri wake, na kiwango cha dunia alichofikia kuna mashaka makubwa juu yake, sishangazwi naye”.

Sean Dyche aridhishwa na timu yake
Bosi wa Burnley Sean Dyche ameonyesha matumaini yake kuwa kikosi chake kitarudia katika njia yao ya ushindi watakapokuwa nyumbani dhidi ya Tottenham wikiendi hii.
Burnley kwasasa iko katika nafasi salama ya 13 katika msimamo wa ligi ya Premier baada ya kukusanya alama 32 kwa michezo 29 waliyocheza, ambapo Dyche ameonyesha kuridhishwa na hali ya mambo katika kampeni ya msimu huu.
Kwenda michezo 7 bila ushindi ilikuwa ikionyesha kuwa klabu hiyo iko katika hatari ya kudondoka zaidi katika msimamo wa ligi na ushindi katika michezo yake mingi ukitokea katika dimba la nyumbani, Turf Moor.
Ni vilabu viwili tu vya Chelsea na Tottenham vyenye rekodi nzuri katika uwanja wa nyumbani msimu huu, hali inayomfanya Dyche kuliambia gazeti la Telegraph na hapa namnukuu “kwa ujumla naridhishwa, hatujaribu na tunashinda alama, lakini inatosha kusema tuko katika muonekano mzuri.

Ageuro kusalia Manchester City msimu ujao
Na Sergio Aguero anasema lengo lake ni kusalia Manchester City licha ya ripoti za karibuni kueleza kuwa ataihama klabu hiyo mwisho wa msimu.
Aguero amejikuta katika benchi kwa wiki kadhaa msimu huu kufuatia kuwasili kwa Gabriel Jesus ambaye alianza kuonyesha mabadiliko ndani ya klabu hiyo akifunga magoli kabla ya kupatwa na majeraha ambayo yatamuweka nje ya kikosi hadi mwisho wa msimu.
Licha ya kuwa katika kiwango kizuri na kufunga magoli muhimu katika kikosi cha City katika siku za karibuni amekuwa akiandikwa na tetesi kuzidi kuchukua nafasi kuwa huenda akaihama klabu yake.
Aguero mwenye mkataba na Etihad hadi 2020, ameiambia redio moja ya nchini Hispania Onda Cero kuwa ana miezi mitatu ya kuonyesha ubora wake na kama siku zote amekuwa akisema basi isubiriwe mwezi June.
Hivi karibu Manchester City ilitangaza kuwa itasalia na Aguero, ingawa bado haijatoa taarifa za kimaandishi.