CAF yabariki mabadiliko ya tarehe za mashindano yake ya vilabu, fainali sasa kupigwa Mei

Junior Binyam mkurugenzi wa habari wa CAF

Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF) limeweka wazi jinsi tarehe za mashindano yake ya ngazi za vilabu yatakavyo anza kubadilika ndani ya mwaka 2018.

CAF imeelezea namna mashindano hayo yatakavyo endeshwa kati ya miezi ya Agosti, Septemba hadi Mei lakini si kwa lengo la kufananisha tarehe ya mashindano ya vilabu Ulaya.

“Mabadiliko haya si kwa lengo la kuyapeleka sambamba na mashindano ya vilabu vya Ulaya isipokuwa ni angalau tuwe sawa na Ulaya kwa asilimia 75 ” Amesema mkurugenzi wa mawasiliano wa CAF Junior Binyam.

“Hii pia itaruhusu tuwe na kipindi cha usajili wa wachezaji wa mashindano ya CAF ambacho kitalingana na nchi nyingine ambazo tayari zinatumia kipindi hicho.

“Pia itarekebisha mambo kwenda katika muda mpya wa mashindano ya kimataifa, ambayo ni mataifa ya Afrika”

Kuanzia 2019 Michuano ya mataifa ya Afrika yatakuwa yakifanyika mwezi Juni na Julai tofauti na ilivyozoeleka kwa tarehe za mwezi Januari na Februari.

Hapo awali mashindano ya klabu bingwa Afrika na ile ya kombe la shirikisho yalikuwa yakifanyika katika kalenda ya ndani ya mwaka kama ilivyokuwa mwaka huu 2017 ambapo yalifanyika kuanzia Februari hadi Novemba.

Kwa msimu wa mwaka 2018 mashindano yataendelea kufanyika kwa tarehe za sasa na yataanza tena Disemba kwa msimu mpya hadi Mei 2019.
Dirisha jipya la utaratibu mpya wa mashindano yote mawili litafunguliwa kati ya Septemba na Oktoba 2019 na kumalizika Mei 2020.

Mabadiliko haya ya tarehe katika mashindano yote ya vilabu yamepitishwa katika mkutano wa kamati ya utendaji wa mwezi Julai nchini Morocco, kufuatia mjadala mkubwa ulio husu hatma ya mchezo wa soka barani Afrika.

Be the first to comment

Leave a Reply