Kamati ya taifa Stars ni ya vikao vya kahawa

Yapo mambo ambayo ukiwaza sana kwa muda mrefu kwa utulivu mkubwa ndio unaweza kupata majibu yake kwa urahisi zaidi lakini kuna mengine huitaji fikra ndefu ili kupata majibu yake.

Binafsi katika hili sikutumia muda mwingi kupata majibu yake isipokuwa ni kutumia kumbukumbu ya kile ambacho kimetokea huko nyuma na njia ambzo tunajaribu kupita sasa kufanana na yale yale ya kipindi kile.

Naelewa kuwa si kila mtu kabarikiwa muono na uwelewa sawa katika kutafuta mafanikio lakini kuna mengine yanakuja kwa kujifunza kutokana na makosa na kujirekebisha kutokana na makosa hayo aidha kwa kuuliza au kufanya utaratibu mwingine ambao utafanana na wengine ambao wamefanikiwa.

Jitihada za Tanzania katika kuhakikisha timu ya taifa ya soka taifa stars inapenya katika hatua za awali na kutinga hatua ya makundi na hata kutoka katika hatua ya makundi na kutinga katika fainali za mataifa ya Afrika au kombe la dunia mara zote zimekuwa zikigonga mwamba kutokana na ukweli kwamba Tanzania haitaki kujifunza namna ambavyo mataifa mengine yamekuwa yakijipanga na kampeni hizo na hatimaye kufanikisha malengo yao.

Ukweli ni kwamba kampeni hizi kwa Tanzania zinawaweka pembeni wadau wa kweli wamchezo huo ambao wana sifa, ujuzi, uweledi na uzoefu wa kukabiliana na wapinzani ambao kwa namna moja ama nyingine wanajua namna ya kuruka vikwazo na vizingiti katika kampeni kama hizi.

Hapa niseme wazi tu kuwa jaribio la Jamali Malinzi katika kusaka nafasi ya Tanzania kucheza kombe la Dunia 2018 nchini Urusi na kufuzu fainali za mataifa ya Afrika ni sawa na ule msemo wa zamani kidogo wa kucheza makida wenye mpira wao wako nje.

Rais Malinzi ameunda kamati ya Stars ambayo inaongozwa na Mwenyekiti Farough Baghouzah na wajumbe wake Teddy Mapunda (Katibu), Wajumbe ni Juma Pinto, Michael Wambura, Iman Madega, Salum Abdallah na Isaac Chanji. Hili ni jambo ambalo anastahili kupongezwa katika jitihada zake za kuona kuna haja ya kuunganisha nguvu katika kusaka mafanikio katika kampeni mbili za Stars za kombe la dunia na AFCON.

kamati
Hili si jambo geni kwa watu wa mpira ambao wanatunza vema kumbukumbu zao vizuri kwani wakati wa awamu ya pili ya uongozi wa serikali Rais Ally Hassan Mwinyi aliwahi kuunda kamati kama hiyo iliyokuwa ikiitwa kamati ya SAIDIA TAIFA STARS ISHINDE ambayo iliundwa mwaka 1994 na ilikuwa ikiongozwa na Dr Reginald Mengi mwenyekiti wa makampuni ya IPP na wajumbe wake walikuwa ni pamoja na mwenyekiti wa chama cha soka nchini FAT alhaji Muhidini Ndolanga, Kuwayawaya. S Kuwayawaya aliyekuwa mbunge wa Dodoma njini.

Miongoni mwa wajumbe wengine ni pamoja na Brigedia Moses Mnauye, waandishi wa habari na wapiga picha mashuhuri Richard Mwaikenda na Muhidini Issa Michuzi.

Mwaka 1994: Rais Ali Hassan Mwinyi akiwa na wajumbe wa kamati ya Saidia Taifa Stars ishinde Ikulu jijini Dar es salaam baada ya timu hiyo kunyakua ubingwa wa Chalenji. Kutoka kulia mstari wa mbele ni Issa Michuzi (Ankal), Brigedia Moses Nnauye (RIP), mwenyekiti wa FAT wakati huo Alhaj Muhidin Ndolanga, Rais Mwinyi, Waziri wa Elimu na Utamaduni Profesa Philemon Sarungi wakati huo , Mwenyekiti wa kamati hiyo na Mwenyekiti wa makampuni ya IPP Reginald Mengi, Mbunge wa Dodoma Kuwayawaya S. Kuwayawaya na Kamanda Richard Mwaikenda. Toka wakati huo Taifa Stars haijashinda kombe lingine lolote.
Mwaka 1994: Rais Ali Hassan Mwinyi akiwa na wajumbe wa kamati ya Saidia Taifa Stars ishinde Ikulu jijini Dar es salaam baada ya timu hiyo kunyakua ubingwa wa Chalenji. Kutoka kulia mstari wa mbele ni Issa Michuzi (Ankal), Brigedia Moses Nnauye (RIP), mwenyekiti wa FAT wakati huo Alhaj Muhidin Ndolanga, Rais Mwinyi, Waziri wa Elimu na Utamaduni Profesa Philemon Sarungi wakati huo , Mwenyekiti wa kamati hiyo na Mwenyekiti wa makampuni ya IPP Reginald Mengi, Mbunge wa Dodoma Kuwayawaya S. Kuwayawaya na Kamanda Richard Mwaikenda. Toka wakati huo Taifa Stars haijashinda kombe lingine lolote.

Kamati hiyo ilifanya kazi nzuri sana chini ya mzee Mengi kwani ilitimiza jukumu walilokusudia kwa Stars kushinda kombe la Chalenji.

Wakati fulani waziri wa habari utamaduni na michezo akiwa ni Mohamed Seif Khatib, iliwahi kuundwa kamati kama hiyo na hata mwaka 2013 waziri wa habari utamaduni na Michezo Dr Fenera Mukangara naye aliunda kamati kama hiyo kwa kutumia jina hilo hilo kwa ajili ya kusaidia timu ya taifa kufuzu fainali za kombe la Dunia nchini Brazil 2014.

Kamati ya Dr Fenera ilikuwa ikiongozwa na mwenyekiti mheshimiwa mbunge wa Singida mjini Mohamed Dewji, Teddy Mapunda, Dr Ramadhani Dau (Mkurugenzi Mtendaji NSSF), Dioniz Malinzi (Mwenyekiti BMT), Abji Shabir (New Africa Hotel), George Kavishe (TBL), Mohamed Raza (Mfanyabiashara na mwakilishi wa jimbo la Uzini-Zanzibar).

Wengine ni Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)Jamali Malinzi, Joseph Kusaga (Clouds), Marehemu Kapteni John Komba aliyekuwa mbunge Mbinga Magharibi na mheshimiwa Zitto Kabwe wakati huo akiwa mbunge wa Kigoma Kusini.

Baadhi ya wajumbe wa kamati ya saidia Stars ishinde 2013
Baadhi ya wajumbe wa kamati iliyopita saidia Stars ishinde

Kamati iliyoundwa na Dr Fenera iliundwa wakati tayari Stars ikiwa na matokeo mazuri katika kundi lake la ‘C’ ambalo lilikuwa na timu nne nyingine ni Ivory Coasta, Morocco na Gambia. Baada ya michezo mitatu ya mzunguko wa kwanza tayari Stars ilikuwa na pointi 6 nyuma ya waliokuwa vinara wa kundi Ivory Coastal walikuwa na pointi saba, Morocco walikuwa na pointi mbili huku Gambia wakishika mkia kwa kuwa na pointi moja.

Hata hivyo licha ya kamati hiyo kuundwa mambo yalizidi kuwa mabaya na Stars haikufua dafu badala yake ilifungwa michezo yake mitatu yote iliyosalia katika kundi, mbaya zaidi hata Morocco tuliokuwa tumewaacha mbali kwa pointi nne walitupita na mwisho wa siku baada ya michezo yote sita kumalizika msimamo wa kundi C ukaonyesha wa kwanza Ivory Coastal walikuwa na pointi 14, wakifuatiwa na Morocco waliovuna pointi 9 na Stars kusalia na pointi zake 6 huku Gambia wakishika mkia kwa pointi 4 wakipata ushindi pekee dhidi ya Tanzania.

Hebu tujiulize kama watanzania ambao kila mmoja ana kiu kubwa na mafanikio ya timu ya taifa, hivi hizi kamati zinaundwa na watu wenye uweledi wa kisoka?. Hivi kinachotafutwa hapa ni kuitoa Algeria au ni kamati za kukutana hotelini na kunywa chai pamoja?

Kitu cha kushangaza ni kwamba kamati iliyoundwa na Jamali Malinzi wiki iliyopita imeivunja rasmi kamati ya Dr Fenera Mukangara ambayo imehudumu kwa miaka miwili tu na wajumbe wake baadhi bado wapo ukiachilia mbali maheremu Kapteni Komba ambaye ametangulia mbele ya haki(RIP). Ni vema Malinzi angeweka wazi madhaifu ya kamati ya Dr Mukangara kabla ya kuunda hii ya Farough Baghouzah na kutoa majibu ya maswali mengi ambayo yanaweza kuibuka kutokana na kile ambacho kinaendelea hivi sasa.

Hivi ni nini hasa ambacho kinatakiwa kwa sasa ni kamati au mkakati wa ushindi dhidi ya Algeria hapa nina maana ya kwamba mkakati si lazima kuundwa kamati. Mbaya zaidi ni baada ya vikao mara mbili katika hoteli ya Serena viongozi wa kamati hiyo wamejitokeza hadharani baada ya uteuzi wao wakiwa na kamati nyingine ndogo ndogo ambazo kimkakati hazina ulazima na pengine kamati hizo nazo zitahitaji vikao vya mara kwa mara na posho za vikao ili kufanya kazi zao ambazo ukiangalia ni kazi za kamati ya utendaji ya shirikisho la soka.

Kamati mpya ya Stars iliyo chini ya Farough Baghouzah imeelezewa kuwa itashungulika na Kuimarisha huduma kwa wachezaji, Uhamasishaji na Masoko, Kuhamasisha wachezaji na Kuandaa na kusimamia mkakati wa Ushindi.

Ingekuwa bora ikatambulishwa kuwa ni kamati ya kuchangisha pesa nadhani watanzania wangeelewa haraka zaidi kuliko ilivyotambulishwa na Rais Malinzi, kabla ya kujimbulisha yenyewe kwa waandishi wa habari na kuongeza kamati ndogo ndogo ambazo kimtazamo wa haraka ni kwamba kamati zote hizo ndogo ndogo zitakuwa zinafanya kazi inayofanana.

Tukianza na hilo la kuimarisha huduma kwa wachezaji, si kweli kwamba mchezaji ili afanye vizuri anahitaji kuundiwa kamati ya kumuhudumia ili aweze kufanya vizuri kama Programu ya kocha haitatekelezwa vema na kama atakosa maandalizi muhimu ya kiufundi na kisaikolojia.

Nini maana ya huduma kwa mchezaji? hivi mchezaji anapaswa kuhudumia na nani? Walipocheza na Malawi na timu kuibuka na ushindi nani awahudumia je aliweza au hakuweza na kama aliweza kamati hiyo inayoundwa ya nini?

Nimejaribu kutafuta kutoka kwa wenzetu wa nje kujua kama kuna utaratibu wa kuundwa kamati kama ya kwetu sijaona popote zaidi ni kambi yenye kila kitu na Programu iliyokamilika bila kusahau posho za wachezaji.

Suala la Uhamasishaji na masoko kuundiwa kamati nashindwa kuelewa, hivi Marcio Maximo aliwezaje yeye kama yeye jeshi la mtu mmoja kujenga hamasa ya kila mtanzania na kuunganisha nguvu zao na kujenga uzalendo miongoni mwao kisha kujaza uwanja wa taifa watu wakishangilia mwanzo mwisho.

Malinzi ukitaka kampeni hii ya uhamasishaji ifanikiwe hakikisha kila mtanzania anaingia uwanjani siku ya mchezo dhidi ya Algeria.

Hilo litafanikiwa kwa kualika kiongozi mkubwa kutoka serikalini au mstaafu ambaye anapendwa na watanzania na anaweza kuwa alhaji Ally Hassan Mwinyi, ambaye kwasasa anaweza kufuta msemo wake wa Tanzania ni kichwa cha mwendawazimu na pia ukamualika rasmi kufika uwanjani kama mgeni wa heshima.

Wadau pekee wa kuhamasisha stars kufanya vizuri ni wachezaji wenyewe na sio wafanyabiashara ambao wamejiunga kama kikundi cha kirafiki ambao wanakutana Serena hoteli kwa vikao vya kamati jambo ambalo hata Malinzi mwenyewe na kamati yako ya utendaji hawakutani katika mazingira hayo kwa vikao vya mpira, mbaya zaidi hata mkutano na waandishi wa habari unaitishwa ndani ya hoteli hiyo.

Jambo la kujiuliza ni kwamba nani analipa posho za kikao vyao? Kama ni TFF kwanini ifanyike hivyo kwa kamati ndogo kama hiyo ilhali katika jengo la ofisi za TFF kuna chumba kikubwa cha mkutano na kuna kiyoyozi kinapuliza?

Hata kama wanajitolea pesa zao za mifukoni sasa inakuaje wanataka Stars ichangiwe ilhali wao wanauwezo wa kukutana Serena. Katika hali ya kawaida ni nani atachangia mia mbili yake ambayo itachangia vikao vya Serena badala ya chumba cha bure cha TFF? Hi ni dhihaka na ndio maana nathubutu kuita kamati ya vikao vya kahawa na chai kwenye migahawa mikubwa.

Ingefaa basi wanakamati hao wachangie kambi ya Stars kwa kutoa pesa na vitu mbalimbali ambayo ni mahitaji muhimu kwa wachezaji kuliko vikao vya kahawa ambayo mwisho wa siku ni aibu baada ya mchezo dhidi ya Algeria.

Kuandaa wachezaji Katika hali ya kimchezo zaidi vizuri kuwashirikisha wachezaji wa Tanzania waliowahi kucheza soka katika miaka ya nyuma kwa mafanikio makubwa kama vile Sunday Manara, Leopard Tasso, Mtemi Ramadhani, Peter Tino, Zamaoyoni Mogella, Seif Bausi na hata mkuu wa mkoa wa Manyara Joel Bendera ambaye Stars aliyokuwa kocha ilikwenda Lagos katika fainali za mataifa ya Afrika 1980 kwa kutaja wacheche tu, kwa lengo la kujenga saikolojia ya wachezaji kabla ya mchezo mkubwa kama huo hao wanaweza.

Aliyekuwa Rais Kabla ya Malinzi, Leordigar Tenga alitengeneza rasilimali watu, alimjenga vizuri alhaji Ahmed Msafiri Mgoyi katika kufahamu vizuri fitna za kimataifa hususani katika soka barani Afrika, huyu ni mjumbe wa kamati ya utendaji ya TFF ambaye tayati ni mratibu wa Stars kwasasa nadhani anatosha kuungana na wajumbe wako wa kamati ya utendaji kuweka mkakati imara usiokuwa na gharama na kuunganisha mambo na benchi la ufundi ambalo liko chini ya Charles Bonface Mkwasa.

Kwa mtazamo wangu sura nyingi zinazoonekana katika kamati ya Stars na hata wale wachache waliongezwa katika kuunda kamati ndogondogo ni za watu maarufu ambao kwa kweli naona wanakutana kwa vikao vya kirafiki vya Breakfast, Lunch na Dinner na si kujenga maandalizi ya ushindi dhidi ya Algeria.

Nampongeza aliyetoa wazo la kuundwa kwa kamati hii hakukosea kutoa wazo hilo ambalo kimsingi lilihitaji fikra zaidi katika muundo wa kamati na wajumbe stahiki.

Baniani mbaya kiatu chake dawa kauli mbiu inavutia “NCHI YETU, TIMU YETU, TAIFA LETU, USHINDI WETU”