Klabu ya Simba yaingia mkataba na SportPesa

Na Zainab Nyamka, Globu ya Jamii.

Kampuni ya SportPesa imeingia mkataba wa miaka mitano wa kuidhamini klabu ya Simba ukiwa na thamani ya Bilion 4.9 .

Kampuni hiyo inayojishughulisha na masuala ya michezo ya bahati nasibu nchini Kenya imeweza kuingia nchini Tanzania na kuja kufanya uwekezaji kwa klabu mbalimbali za mpira wa miguu.

Utiaji saini wa makubaliano ya mkataba huo umefanyika jioni hii katika ukumbi wa Uwanja wa Taifa na kushuhudiwa na wadau mbalimbali wa mpira nchini.

Rais wa Klabu ya Simba Evance Aveva amesema mkataba huu utaweza kuwasaidia katika kuendelea kutoa hamasa kwa timu yao kufanya vizuri zaidi.

Kwa upande wa Mkurugenzi wa SportPesa nchini Abbas Tarimba amesema kuwa wamefurahi sana kuingia mkataba na Timu ya Simba na mkataba wao utakuwa katika hatua tofauti kulingana na makubaliano waliyoyaingia.

Amesema kwa mwaka wa kwanza Klabu ya Simba watapata milioni 880 na katika miaka mitatu inayofuata watapata nyongeza ya asilimia 6 huku mwaka wa mwisho wa mkataba huo klabu hiyo itafaidika kwa kupata bilioni 1.08.

Mbali na hilo Tarimba amesema kuwa klabu ya Simba itafaidika kwa kupata fedha mbalimbali kama hamasa iwapo wataweza kupata ubingwa kwa kupewa bonus ya milioni 100 au kushiriki michuano ya kimataifa.

Kabla ya utiaji saini wa mkataba huo Simba iliweza kutoka na ushindi wa goli 2-1 dhidi ya stand United magoli yakifungwa na Laudit Mavugo na Juma Luizio huku la Stand likifungwa na Kasim Selembe.
chanzo