Makala Na Uchambuzi

Hivi ni kweli mpira pesa? Udhamini wa BG Tanzania na Binslum&tires Ndanda fc ndiyo timu iliyopoteza michezo mingi ligi ya Vodacom

Wakati ligi kuu ya soka Tanzania Bara ikiingia katika mapumziko baada ya kukamilisha raundi saba za awali, timu Ndanda fc ya mtwara ‘wazee wa kuchele’ wanapaswa kujitathmini upya juu ya mwenendo wao mbaya wa ligi hiyo ukiwa ni msimu wao wa kwanza ndani ya ligi hiyo.

Ndanda ambayo ilianza ligi kwa ushindi wa kishindo wa bao 4-0 dhidi ya Stand United ya Shinyanga imekuwa na mdororo wa matokeo mpaka kufikia sasa ikiwa imekubali kufungwa michezo mingi zaidi ukilinganisha na timu nyingine zinazo shiriki ligi hiyo.

Timu hiyo inayotokea mkoani Mtwara imeruhusu kufungwa jumla ya michezo mitano huku nyavu zao zikiwa zimetikiswa mara 12 ambayo ni zaidi ya timu zote.

Pamoja na kupata ushindi dhidi ya bingwa mtetezi Azam fc ya jijini Dar es Salaam mchezo uliofanyika katika uwanja wa Nangwanda Sijaona, bado Ndanda imeendelea kupoteza mchezo mwingine dhidi ya JKT Ruvu kwa bao 2-0 mchezo uliofanyika jana uwanja wa Azam Complex Chamazi.

Huu si mwenendo mzuri hata kidogo kwa timu hiyo, kama inataka kusalia katika ligi msimu ujao italazimika kufanyika kazi kubwa ya kimakusudi kwa kushirikiana na wadau wa mkoa wa Mtwara kubadilisha hali hiyo.

Pamoja na kumtimua kocha wao Dennis Kitambi na msaidizi wake kocha wa makipa Mohamed Mwarami, bado timu hiyo imekuwa na matokeo ya kusuasua.

Licha ya udhamini mzuri wa makampuni mawili ya Binslum & tires pamoja BG Tanzania, ukiachana na fedha za mdhamini mkuu wa ligi Vodacom kwa pamoja na fedha za haki ya matangazo kutoka Azam TV bado hali si shwari kwa timu hiyo inapokuwa uwanjani, swali nini tatizo kwao?

Ndanda inashika nafasi ya nafasi ya 13 katika msimamo wa ligi kuu Tanzania Bara baada ya michezo saba ikiwa na alama 6 ilizopata kwa Stand United na Azam fc, ikiwa haijakwenda sare hata mchezo hata mmoja ikifungwa michezo mitano. Kauli mbiu ya Ndanda Kuchele sasa imepoteza maana na hata kufikia hatua ya kubadilika na kuwa Ndanda kwa roho safi.

Be the first to comment

Leave a Reply