Nje ya kambi wachezaji wa Arsenal wamtetea Bosi wao

Wachezaji wa Arsenal wanaonekana kuitumia nafasi ya mapumziko ya kimataifa kuonyesha ni kiasi gani wanamkubali meneja wao Arsene Wenger aliye katika presha kubwa kuwahi kutokea tangu alipojiunga na klabu hiyo.

Karibu kila siku ndani ya wiki hii, wachezaji mbalimbali wamekuwa wakinukuliwa wakisema wanataka Wenger kusaini mkataba mpya wakati mkataba wake wa sasa ukitarajiwa kufikia tamati mwisho wa msimu huu.

Kutoka kwa Olivier Giroud na Laurent Koscielny katika kambi ya timu ya taifa ya Ufaransa, Hector Bellerin na Nacho Monreal walioko katika kambi ya timu ya taifa ya Hispani, Alex Iwobi nchini Nigeria na Granit Xhaka aliyeko nchini Switzerland, wamekuwa wakinukuliwa wakimzungumzia bosi katika hali chanya na wakimtetea.

Kitu kibaya ni namna ambavyo wamekuwa wakishindwa kuwasilisha ubora wao kiwanjani. Kama wachezaji wa Arsenal wanataka kweli Wenger asaliye Emirate, wanapaswa kudhihirisha kwa ushindi na sio maneno.

Kwa upande wake Koscielny alinukuliwa akisema, nafasi ya Wenger iko katika kitisho kwa sehemu moja kwasababu wachezaji wamemuangusha.

“tuko katika hali ngumu lakini sio wajibu wake pekee,” Amesema Koscielny

“ni sisi, kiwanjani tunatakiwa kufanya zaidi”

Inawezekana Wenger akasalia kwa miaka miwili zaidi bila kujali nini kitatokea kati ya sasa na mwezi Mei. Lakini endapo hatma yake itategemea wanavyotaka mashabiki kabla ya msimu kumalizika, ni wachezaji pekee ambao wana uwezo wa kuokoa kibarua chake. Kuiambia dunia kwa kiasi gani wanamtaka Wenger kusalia haina maana, vinginevyo waanze kucheza inavyotakiwa na kupata matokeo.

Kwa kuzingatia matokeo ya mchezo dhidi ya West Brom ambapo Arsenal ilifungwa 3-1, wachezaji wachezaji wa klabu hiyo hawaonekani kuguswa na hilo kwamba kila matokeo mabovu yanapotokea basi yanazidi kuongeza presha kwa meneja wao.