Pochettino afurahia matokeo ya sare dhidi ya Real Madrid

Meneja wa Tottenham Hospurs Mauricio Pochettino afurahishwa na sare dhidi ya Real Madrid ugenini.

Maurcio Pochettino amefurahishwa na sare ya Tottenham dhidi ya mabingwa watetezi Real Madrid, akisema mechi hiyo imeonyesha kuwa timu yake inaweza kushindana katika kiwango cha hali ya juu.

Tottenham waliondoka Santiago Bernabeu wakiwa na pointi moja baada ya kuwang’ang’ania mabingwa hao kwa sare ya 1-1 Jumanne.

Ilikuwa ni mechi ya kukata na shoka baina ya timu hizo mbili za Kundi H baada ya goli la Raphael Varane la kujifunga kufutwa na Cristiano Ronaldo kipindi cha kwanza.

Jitihada za Madrid kutafuta goli la pili zilizuiliwa na nahodha wa Tottenham na mlinda mlango Hugo Lloris, wakati Harry Kane na Spurs walizuiliwa kufunga na Keylor Navas.

Meneja wa Tottenham hakuwa na cha kusema ila kuwasifia wachezaji wake baada ya mechi katika jiji kuu la Hispania, akisema: “Najivunia na nina furaha sana. Kila mmoja alitaka kushindana na kuonyesha kuwa tunaweza kushindana katika kiwango cha hali ya juu. Nimefurahi sana.

“Ufanisi ulikuwa mzuri sana. Nampongeza kila mmoja kwa sababu ilikuwa nzuri sana na mashabiki wetu walikuwa pamoja nasi, siwezi kuamini na [nasema] asante sana kwa kutuunga mkono na kutusaidia. Ulikuwa ni mchezo wa kuvutia sana.”

Pochettino aliongeza: “Daima huwa nawaambia wachezaji wangu kuwa ni mechi ya kufurahia – chezeni, kimbieni, muwe huru, jaribuni kucheza kwani kucheza katika kiwango hicho ndiyo ndoto yetu, mara zote, tangu nilipoanza miaka mitatu iliyopita, kucheza Ligi ya Mabingwa, dhidi ya Real Madrid tena ndani ya Bernabeu. Soka ni raha.

“Kuwa jasiri ni muhimu sana. Kama unataka kushinda na kama unahitaji kukuza kiwango chako, jifunze kuimarika, ni muhimu sana kuwa shupavu.

“Naam unapocheza ni lazima utunze utambulisho wako na ushindane kweli. Michuano ya Ligi ya Mabingwa msimu uliopita haikuwa vizuri kwetu kwani hatukushindana vema, lakini katika mechi hizi tatu [dhidi ya Borussia Dortmund, APOEL na Real Madrid] Nadhani timu imepevuka, na hatuchezi tu, bali tunashindana kweli na hilo ndilo jambo muhimu.”

“Tupo katika nafasi nzuri sana,” aliendelea. “Tuna pointi saba sawa na Madrid. Inapendeza. Changamoto yetu ni kufika hatua nyingine na tumefurahia matokeo. Nafurahi kwa ajili ya mashabiki wetu, kwa ajili ya timu na kikosi chetu pia. Nimejawa na furaha tele.”

Be the first to comment

Leave a Reply