Raundi ya 30 Ligi ya Premier ilivyokuwa

Tuanzie katika dimba la Anfield, Liverpool iliongezea matumaini ya kuendelea kusalia katika kundi la timu nne bora baada ya kuwatandika Everton mabao 3-1 katika Champions League.
Sadio Mane aliwapa Liverpool bao la mapema kufuatia ushirikiano mzuri na Roberto Firmino.
Bao la pili lilifungwa na Philipe Coutinho baada ya kuwabwaga wachezaji wawili wa Everton.

Kule Emirates, Arsenal ilijitahidi mara mbili ikasawazisha na kutoka sare ya mabao mawili na Manchester City, matokeo ambayo yanaiweka nyuma ya City kwa pointi saba.
Kiungo wa mbele Leroy Sane, aliwafungia wageni bao la kwanza dakika tano baada ya kuanza kwa mechi, lakini Theo Walcott akawaokoa Arsenal na kusawazisha bao hilo.
Hata Sergio Aguero alikifungia kikosi cha Pep Guardiola takriban dakika mbili baada ya kuanza kwa kipindi cha pili.
Naye Shkodran Mustafi alitumia fursa ya kona iliyochongwa na Mesut Ozil na kusawazisha mabao 2.
Huku hatma ya meneja Arsene Wenger ikiwa haijulikani, sare hiyo inaicha Arsenal katika nafasi ya sita licha ya kubaki na mechi kadha za kucheza.

Swansea City na Middlesbrough zimeshindwa kufungana na kila upande kuambulia alama moja yenye pumzi ndogo katika kujaribu kujiokoa na balaa la kushuka daraja.
Licha ya kila upande kutengeneza nafasi na nyingine za wazi lakini ugumu wa mchezo ulifanya matokeo kusalia 0-0 hadi dakika 90 za mchezo.
Leroy Fer wa Swansea alipata nafasi nzuri ya kuandikisha goli katika dakika ya 89 lakini mpira aliopiga ulipaa juu ya lango la Middlesbrough huku nao Middesbrough kupitia kwa Rudy Gestede katika dakika za nyongeza mpira alishindwa kuukwamisha mpira wavuni baada ya kupata nafasi ya mpira wa kichwa.
Swansea wamesalia na alama moja juu ya timu 3 za mwisho ilhali Middlesbrough ikishika nafasi ya 19 na ikidaiwa alama 5 kujiondosha katika eneo la kushuka daraja.

Tottenham imefanikiwa kupunguza wigo wa alama na vinara Chelsea hadi kusalia alama 7 baada ya kufanikiwa kuidhoofisha Burnley kwa matokeo ya ushindi wa goli 2-0 katika mchezo uliopigwa katika dimba la Turf Moor.
Licha ya kufanya mashambulizi yasiyozaa mabao, Spurs haikukata tamaa iliendelea kuongeza presha katika goli la Burnley na hatimaye kupitia kwa Eric Dier ilifanikiwa kuandika goli la kwanza baada ya walinzi wa Burnley kushindwa kuokoa mpira wa Christian Eriksen.
Vincent Janssen alipata nafasi ya kuanza katika ligi ya Premier tangu kuingia mwaka 2017, hata hivyo aliumia na nafasi yake kuchukuliwa na Son Heung-min ambaye aliandikisha goli la pili la Spurs baada ya kupokea pasi nzuri ya Dele Alli katika dakika ya 77 ya mchezo.

Katika dimba la Stamford Bridge, Chelsea ambayo inaongoza ligi hiyo ilisimamishwa kasi yake na Crystal Palace pale ilipokubali kichapo cha bao 2-1.
Licha ya kikosi hicho cha Antonio Conte kushinda michezo 10 iliyopita katika dimba hilo tangu Septemba 16 lakini mara hii ilikwaa kisiki cha Palace.
Hata hivyo Chelsea ndio waliokuwa wa kwanza kupata goli la uongozi kupitia kwa Cesc Fabregas aliyetumia vema mpira wa krosi wa Eden Hazard dakika 5 tangu mchezo huo kuanza.
Wilfried Zaha alisawazisha goli hilo baada ya kufanya jitihada binafsi huku akizongwa na walinzi wa Chelsea na sekunde 91 baadaye alitengeneza nafasi kwa Christian Benteke na kuandikisha goli la pili na la ushindi kwa wageni.

Ikiwa katika dimba lake la KCOM, Hull City ilipata pumzi mpya ya kuepuka kushuka daraja baada ya kuifunga timu ngumu ya West Ham bao 2-1.
Wageni ndio waliokuwa wa kwanza kupata goli la utangulizi kupitia kwa Andy Carroll ambaye kwake lilikuwa ni goli lake la 50 katika ligi ya Premier, lakini hata hivyo magoli ya kipindi cha pili ya Andrew Robertson na Andrea Ranocchia yaliamua matokeo ya mchezo huo.
Ushindi huo umeifanya Hull City kufikisha alama 27.

Katika dimba la King Power, Bosi wa muda wa Leicester City Craig Shakespeare ameendelea kupata matokeo ya asilimia 100 katika michezo yake 4 ya kwanza tangu alipochukua mikoba ya Claudio Raniaeri na mara hii akiishinda Stoke City kwa bao 2-0.
Alikuwa ni Wilfred Ndidi aliyeandika goli la uongozi kwa shuti la umbeli wa yadi 25 lililomshinda golikipa wa Stoke Lee Grant na kutua juu kwenye kona ya goli.
Goli la pili lilizamishwa kambani na Jamie Vardy.
Matokeo hayo yana maana kuwa Shakespeare aliyeanza kukinoa kikosi cha Leicester mwezi February, ndiye meneja wa kwanza Mwingereza kushinda michezo 4 ya kwanza mfululizo katika pili ya Premier.

Katika dimba la Old Trafford, Manchester United yenye shauku ya kutinga katika Top-4 iliacha alama 2 na kuambulia alama moja katika mchezo uliomalizika kwa suluhu dhidi ya West Brom.
Mshambuliaji Marcus Rashford wa United alifanya mashambulizi mara mbili kwa mipira ya kujaribu akiwa mbali lakini mashuti yake yaliokolewa na golikipa wa Brom Ben Foster.
United ilitawala mchezo huku West Brom ikilazimika kutumia wachezaji wake wote kama walinzi.
Nafasi pekee nzuri kwa West Brom ilikuwa pale golikipa David de Gea alipo okoa shuti la kiungo Darren Fletcher.

Kwingineko ni kule Vicarage Road ambako manyigu ya Watford yalipowashambulia paka mweusi wa Sunderland huku goli la Miguel Britos katika kipindi cha pili likitosha kuwapa ushindi wenyeji wa 1-0 wenyeji ambao walimaliza kiu ya kusaka ushindi wa kwanza katika michezo 4 iliyopita.
Ushindi huo umekifanya kikosi cha Walter Mazzarri kusogea hadi nafasi ya 12 katika msimamo wa ligi nao Sunderland wakihitaji alama 7 ili kujinasua katika mkia wa ligi hiyo na ikisaliwa na michezo 9.

Na hatimaye kule St’ Marry ambako mchezo uliozikutanisha Southamton dhidi ya Bounamouth ulimalizika kwa suluhu.
Zikiwa zimesalia dakika 13 kabla ya mchezo huo kumalika Bournemouth ilizawadiwa penati kufuatia Ryan Bertrand kumfanyia madhambi Ryan Fraser lakini penati iliyopigwa na Harry Arter iliota mbawa baada ya mpigaji kutereza wakati akielekea kupiga mpira huo.