Samata na Wanyama waondolewa orodha ya tuzo ya CAF

Shirikisho la soka barani Afrika CAF limetoa orodha ya wachezaji watano watakaoshindania tuzo ya mchezaji bora wa mwaka 2016, kwa wachezaji wa jumla na wachezaji wa ligi za barani Afrika.

Wanaoshindania tuzo ya jumla ya Mchezaji Bora wa Afrika wa Mwaka ni:

  Pierre-Emerick Aubameyang wa Gabon na Borrusia Dortmund
  Riyad Mahrez wa Algeria na Leicester
  Sadio Mane wa Senegal na Liverpool
  Mohamed Salah wa Egypt na Roma
  Islam Slimani wa Algeria na Leicester

Mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania anayechezea soka ya kulipwa Ubelgiji Mbwana Ally Samatta ni miongoni mwa wachezaji 30 waliokuwa wameteuliwa kushindania Tuzo ya shirikisho la soka barani Afrika (CAF) ya Mchezaji Bora wa Afrika katika awamu ya kwanza kabla ya wachezaji hao kupunguzwa hadi watano.

Mkenya Victor Wanyama ambaye kwa sasa anachezea klabu ya Tottenham alikuwa pia ameteuliwa, pamoja na Yannick Bolasie wa DR Congo anayechezea Everton.

Wachezaji watakaoshindania orodha ya Mchezaji Bora wa Afrika wa Mwaka anayecheza ligi za Afrika ni:

  Khama Billiat wa Mamelodi Sundowns na Zimbabwe
  Keegan Dolly wa Mamelodi Sundowns na South Africa
  Rainford Kalaba wa TP Mazembe na Zambia
  Hlompho Kekana wa Mamelodi Sundowns na South Africa
  Denis Onyango wa Mamelodi Sundowns na Uganda

Wachezaji hao waliamuliwa kwa kura zilizopigwa na Kamati ya Wanahabari ya CAF, Kamati ya Kiufundi na Ustawishaji ya CAF na nusu ya wanachama wa jopo la wataalamu 20.
Kwa awamu ya mwisho, kura za makocha wa timu za taifa/wakurugezi wa kiufundi wa mashirikisho 54 ya kitaifa yaliyo wanachama wa CAF pamoja na wanachama washirika – Visiwa vya Reunion na Zanzibar -, kwa pamoja na nsu hiyo nyngine ya wanachama wa jopo la wataalamu 20 zitahesabiwa kuamua washindi.

Mshindi atatangazwa Abuja, Nigeria Alhamisi, 5 Januari 2017.