Wachezaji Nigeria sasa kicheko tu

Wachezaji wa timu ya taifa ya Nigeria (Super Eagles) sasa wanatabasamu baada ya kukabidhiwa malimbikizo ya malipo yao baada ya ushindi wao 2-1 dhidi ya Zambia.

Kwa mujibu wa habari kutoka nchini humo ni kwamba wachezaji wamerudishiwa pesa zao safari, bonasi za mchezo dhidi ya Tanzania mwezi uliopita pamoja na gharama za kucheza michezo miwili ya kirafiki dhidi ya Mali na Luxembourg.

Inakadiriwa kuwa mchezaji aliyecheza michezo yote mitatu ya mwisho amepokea karibu dola za kimarekani 8,000.

Bonasi ya ushindi ya mchezo wa kuwania kufuzu kombe la dunia huko Ndola ndiyo pekee iliyobakia.

Katika mchezo dhidi ya Zambia, Alexander Chuka Iwobi na chipukizi Kelechi Iheanacho walifunga magoli yaliyoipatia Super Eagles ushindi katika uwanja wa Levy Mwanawasa mjini Ndola kabla ya Collins Mbesuma kufunga goli la wenyeji Zambia.

Mwezi Ujao Nigeria watakuwa wenyeji wa Algeria huko Uyo katika muendelezo wa michezo ya kusaka nafasi ya kucheza kombe la dunia 2018.