WWE yapata mwali mpya

Tim Wiese ametangaza rasmi kujiunga na WWE na ataanza mazoezi katika kituo chao cha mazoezi hivi punde. Wiese anadai ya kuwa ilibidi ajiunge na WWE mwaka 2014 ila aliambiwa kwamba anahitaji muda na mazoezi zaidi kabla ya kuchaguliwa kujiunga na WWE.

Wiese alitangaza rasmi kukubali ofa kutoka kwa rais msaidizi wa masuala ya vipaji WWE Paul Levesque ama kwa jina lake maarufu la ‘Triple H’ ya kujiunga na kituo cha WWE Perfomance kilichopo huko Orlando Florida. Akiongea na mtandao wa WWE Triple H alisema Tim ni mkali sana sasa ni zamu yake kuonesha uwezo wake, mambo yakienda vizuri Florida ataingia dimbani.

Tim alisema, “Nimejiandaa sana kwa ajili ya hili na nafurahi sana kupata fursa hii, nitafanya chochote kucheza WWE mwezi Novemba naitaka sana hiyo mechi.” Tim Wiese alikuwa kipa hodari aliyefanikiwa kuchezea klabu kubwa ya Ujerumani ya Werder Bremen kwa miaka mingi, mwaka 2012 alijiunga na klabu ya TSG Hoffenheim kabla ya kustaafu mpira mwaka 2014 kwa sababu ya umri akiwa na miaka 34. Wiese alipata mafanikio makubwa katika mpira na alifanikiwa kuchaguliwa katika kikosi cha Ujerumani kilichoshiriki Kombe la Dunia mwaka 2010.